Lamu,KENYA: Maafisa wa usalama wanaopigana na magaidi wa Al-Shabaab kwenye operesheni inayoendelezwa ndani ya msitu wa Boni Kaunti ya Lamu wamelalamikia ukoesfu wa marupurupu pamoja na mazingira duni ya utendakazi.
Katika mahojiano na wanahabari, maafisa hao wanaohudumu kwenye maeneo ya Milimani, Mararani, Mangai, Basuba, Bodhei na Ishakani mpakani mwa Lamu na Somalia, wanasema kwa zaidi ya miezi sita ambayo imepita hawajapokea marupurupu yoyote licha ya kuahidiwa na serikali kwamba wangelipwa.
Zaidi ya maafisa 3000 wanojumuisha Wanajeshi, GSU, AP, ATPU,na wale wa mpakani (RBPU) wanashirikiana katika kuendeleza operesheni hiyo ndani ya msitu wa Boni.
Operesheni hiyo ya kiusalama ilizinduliwa mnamo Septemba 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo wa Boni.
Kwa upande wake aidha, Mkurugenzi wa Opereshni ya usalama kwenye msitu wa Boni, Joseph Kanyiri, amethibitisha kupokea malalamishi hayo na akaahidi kwamba suala hilo linashughulikiwa na mwafaka kupatikana hivi karibuni.