Washukiwa wa MRC wakana mashtaka mahakamani Mombasa

Washukiwa wa MRC wakana mashtaka mahakamani Mombasa

by -
0 270

Mombasa,KENYA: Washukiwa tisa wa vuguvugu la Mombasa Republican Council-MRC wameshtakiwa katika mahakama ya Mombasa kwa madai ya kuchangisha pesa ambazo zinadaiwa zingetumika kueneza chuki baina ya wanachama wa MRC na makabila mengine chini.

Mahakama imeambiwa kuwa Ali Bandari na wanachama wengine nane, waliandaa mkutano wa harambee, Jumapili iliyopita katika kijiji cha Milalani-Msabweni Kaunti ya Kwale, kwa madai ya kuchangisha pesa za kutumika katika kesi inayomkabili mwenyekiti Ali Bandari katika mahakama ya Kwale.

Wanachama hao walikamatwa na maafisa wa polisi wa Msabweni baada ya chifu wa eneo hilo kuwafahamisha kuhusu mkutano huo uliodaiwa kuandaliwa bila idhini.

Washukiwa wanadaiwa kupatikana na stakabadhi za kueneza chuki ikiwepo wimbo wa vuguvugu hilo, karatasi zilizoandikwa ilani za kutaka makabila mengine kuondoka ukanda wa pwani pamoja na karatasi zilizodaiwa kuwa na maandishi ya kupinga uchaguzi mkuu ujao kufanyika Pwani.

Pia wanadaiwa kupatikana na rekodi za uamuzi wa mahakama kuhusu kesi za MRC na kitabu kilichokuwa kimenakuliwa majina ya wanachama wa vuguvugu hilo, pamoja na idadi ya pesa walizokuwa wakichangisha kuanzia mwezi oktoba hadi mwezi disemba mwaka huu.

Washukiwa wamekana mashtaka hayo mbele ya hakimu Francis Kyambia na akaagiza kila mmoja aachiliwe kwa dhamana ya shilingi laki tano.

Kesi itasikizwa mwezi Machi mwakani.

Imehaririwa na Joseph Jira

Comments

comments

SIMILAR ARTICLES