Wana wa marehemu Ibrahim Akasha wakosa kufika kortini – wakili asema wamelazwa...

Wana wa marehemu Ibrahim Akasha wakosa kufika kortini – wakili asema wamelazwa hospitali

by -
0 291
Wana wa Akasha kuanzia kushoto: Baktash Akasha, Vijaygiri Anandgiri, Gulam Hussein na Ibrahim Akasha wakiwa mahakamani Mombasa.

Mombasa, KENYA: Mahakama ya Mombasa imekataa ombi la kuwakamata wana wawili wa marehemu Ibrahim Akasha waliokosa kukosa kufika kortini Mombasa Alhamisi kufuatia kesi dhidi yao ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Hii ni baada ya mwendesha mashtaka wa Mombasa Alexander Muteti kuiomba mahakama itoe kibali cha kuwakamata na kuwafikisha mahakamani Ijumaa Ibrahim Akasha, Baktash Akasha na mkalimani  katika kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Wakili  wa washukiwa Cliff Ombeta alisema wateja wake walikuwa wadhaifu kiafya na kuwasilisha  mbele ya mahakama stakabadhi kutoka Mombasa Hospital kuthibitisha walikuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.

Lakini mwendesha mashtaka Muteti alidai  stakabadhi hizo zilikuwa ghushi na kusema zimewasilishwa kama njama ya kutaka kesi hiyo isiendelee.

Muteti amesema kesi hiyo imekuwa kortini kwa zaidi ya miaka miwili jambo linaloifanya idara ya mahakama kupoteza hadhi yake.

Mwendesha mashtaka huyo pia ametaka washukiwa wanaodaiwa kulazwa Mombasa Hospital wafanyiwe uchunguzi katika hospitali ya serikali ya Coast General na ripoti iwasilishwe kortini.

Wakili mwingine wa washukiwa Prof. George Wajackoyah alisema hapo awali, hawakukubaliana na tarehe waliyopewa na korti kuhusu siku ya kuamua kesi hiyo na kusema huenda hilo lilisababisha kesi ikose kuendelea Alhamisi.

Pro. Wajackoyah amesisitiza kuwa wateja wake walikuwa wagonjwa na kutaka korti  ifanye uchunguzi kubaini iwapo walilazwa hospitali.

Hakimu mkuu Julius Nang’ea pia ameagiza daktari kutoka mombasa hospital afike kortini kuelezea zaidi kuhusu stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani.

Mahakama imelazimika kuahirisha hadi tarehe 24 mwezi Novemba kutoa uamuzi wa kesi hiyo uliotarajiwa kutolewa Alhamisi.

Uamuzi huo ni iwapo kesi dhidi ya washukiwa isikilizwe nchini Marekani au isikilizwe humu nchini.

Baktash Akasha Abdalla, Gulam Hussein, Ibrahim Akasha Abdalla na Vijagiri Anandgiri Goswami wanahusishwa na ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroine humu nchini na pia nchini Marekani.

Mhariri: Eliakim Mwachoni

Comments

comments

SIMILAR ARTICLES