Masoud Mwahima asema hajutii kuchujwa na chama cha ODM

Masoud Mwahima asema hajutii kuchujwa na chama cha ODM

by -
0 538
Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima akitoka katika ikulu ya rais ya Mombasa. PICHA: HISANI

Mombasa, KENYA: Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amepuuza tangazo la ODM la kumpiga marufuku kutoka chamani, kutokana na hatua yake ya kuasi chama hicho.

Mwahima ameambia Baraka Fm kuwa hajutii na wala hato-omba msamaha kutokana na hatua yake ya kuasi ODM.

Mwahima ni miongoni mwa viongozi 10 waliopigwa marufuku na ODM na ambao inaaminika huenda wakakumbwa na changamoto katika uchaguzi mkuu ujao lakini Mwahima anasisitiza atashinda uchaguzi ujao hata akiwa nje ya ODM.

Baraza la kitaifa la chama cha ODM liliamua kwa kauli moja kuwapiga marufuku chamani wote walioasi ODM na kuunga mkono muungano wa Jubilee.

Katibu wa zamani wa ODM Ababu Namwamba ambaye majuzi alizindua chama chake cha Labour, ni miongoni mwa waliopigwa marufuku kutoka ODM inayoongozwa na Raila Odinga.

Wengine waliochujwa kutoka ODM ni gavana wa Kwale Salim Mvurya, mwakilishi wa wanawake kaunti hiyo Zainab Chidzuga, naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, Mbunge wa Sirisia John Waluke, mbunge wa Nakuru Magharibi Samuel Arama, mbunge mteule Isaac Mwaura, na mbunge wa Mathare Steven Kariuki.

Mhariri: Eliakim Mwachoni

Comments

comments