Meli iliyolipuliwa baharini yatatiza kesi mahakamani Mombasa

Meli iliyolipuliwa baharini yatatiza kesi mahakamani Mombasa

by -
0 484
Meli kwa jina Baby Iris ikilipuliwa katika bahari hindi tarehe 4, Agosti, 2015. PICHA: HISANI

Mombasa, KENYA: Hakimu ambaye amekuwa akisikiliza kesi inayowahusu washukiwa watano wanaohusishwa na ulanguzi wa dawa za kulevya hapa pwani amejiondoa katika kesi hiyo.

Hakimu Julius Nang’ea amejiondoa baada ya kiongozi wa mashtaka Daniel Wamosa  kuwasilisha stakabadhi zinazo-onesha kuwa meli kwa jina Baby Iris ililipuliwa pamoja na dawa za kulevya kufuatia agizo la serikali.

Meli hiyo ilidaiwa kubeba zaidi ya tani 7 za dawa ya kulevya aina ya  heroine za thamani ya shilingi milioni 29.

Hakimu Nang’ea ametaja hatua ya serikali kulipua meli hiyo ilikuwa kinyume cha sheria kwani ingetumika kama ushahidi kortini.

Amesema huenda ilikuwa njama ya kusambaratisha kesi dhidi ya washukiwa watano waliohusishwa na ulanguzi wa dawa hizo.

Pia amesema hatua hiyo imesababisha washukiwa pamoja na mawakili wao kukosa imani na korti na kutaka kesi hiyo isikilizwe na hakimu mwingine.

Meli hiyo ilimilikiwa na raia wa Uingereza kabla ya kulipuliwa  na jeshi la majini katika bandari ya Kilindini Mombasa mwezi Agosti mwaka 2015.

Huku nyuma, serikali iliomba mahakama itoe agizo la kulipua meli hiyo licha ya pingamizi kutoka kwa mawakili wa washukiwa waliosisitiza ingepaswa kutumiwa kama ushahidi.

Lakini meli hiyo ililipuliwa tarehe 4 , Agosti 2015 kabla ya mahakama kutoa uamuzi kufuatia ombi la serikali la kutaka meli hiyo ilipuliwe.

Mahakama ilipaswa kutoa uamuzi huo tarehe 16 Septemba, 2015.

Mhariri: Eliakim Mwachoni

Comments

comments