Mjane wa marehemu Sheikh Aboud Rogo akosa kufunguliwa mashtaka mahakamani

Mjane wa marehemu Sheikh Aboud Rogo akosa kufunguliwa mashtaka mahakamani

by -
0 859
Haniya Said Sagaar , ambaye ni mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo

Mjane wa mhubiri aliyeuawa mwaka 2012 Sheik Aboud Rogo amekosa kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya Mombasa baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi Jumatano jioni.

Haniya Said Sagaar hakufunguliwa mashtaka Alhamisi, baada ya upande wa mashtaka kupitia wakili wa serekali Eugene Wangila kuwasilisha ombi katika mahakama, kutaka mshukiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Nyali kwa siku 14 zaidi ili polisi wafanye uchunguzi kabla ya kumfungulia mashtaka.

Lakini wakili wa mshukiwa Yusuf Abubakar amekosoa ombi hilo la kutaka kuzuilia mteja wake kwa muda zaidi, akisema halina msingi na liko kinyume na katiba.

Abubakar amemtaja mshukiwa kama mama wa familia na ambaye alikuwa tayari kushirikiana na idara ya usalama ili kufanikisha uchunguzi dhidi yake bila kuzuiliwa.

Hakimu Emmanuel Mutunga amesema ombi lililowasilishwa na upande wa mashtaka lilihitaji kushughulikiwa kwa makini na mahakama kabla ya kutoa uamuzi kwa kuwa linahusika na usalama wa nchi.

Mahakama sasa itatoa uamuzi kuhusu ombi hilo Ijumaa.

Haniya Said Sagaar anahusishwa na shambulio lililotokea katika kituo cha polisi cha Central Jumapili iliyopita.

Mahakama imeelezwa kuwa simu ya mshukiwa ilionesha alikuwa akiwasilisna na Tasmin Yakub mmoja wa washukiwa watatu wa kundi la kigaidi waliouawa Jumapili baada ya kuvamia kituo cha polisi cha central.

Polisi hata hivyo wataendelea kuwazuilia hadi tarehe 21 Septemba, washukiwa wengine watatu wanaodaiwa kuwapa hifadhi washukiwa walioshambulia kituo cha polisi.

Washukiwa hao walikosa kufunguliwa mashtaka kwa sababu mmoja wao ana ulemavu wa kuzungumza hivyo atasubiri hadi mtu wa kutafsiri kwa ishara atakapopelekwa mahakamani.

Imehaririwa na Eliakim Mwachoni

Comments

comments

SIMILAR ARTICLES