Polisi washika doria kali mjini Mombasa kabla ya maandamano ya CORD

Polisi washika doria kali mjini Mombasa kabla ya maandamano ya CORD

by -
0 729
Maafisa wa polisi wakishika doria mapema Jumatatu katika bustani ya Uhuru mjini Mombasa kabla ya maandamano ya CORD

Mombasa, KENYA: Maafisa wa kulinda usalama wameshika doria katika bustani ya Uhuru mjini Mombasa kulikotarajiwa kuanza maandamano ya wafuasi wa muungano wa CORD kutaka tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC iondoke mamlakani.

Maafisa hao wa usalama wamejihami kukabiliana na tukio lolote la utovu wa usalama endapo litatokea wakati wa maandamano hayo.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho alitangaza maandamano mjini Mombasa ambayo endapo yatafanyika yatakuwa ya kwanza Mombasa tangu yalipoanza mjini Nairobi majuma matatu yaliyopita.

Hayo yanakuja huku idara ya polisi ikisema haijapokea taarifa yoyote ya kufanyika maandamano na kusisitiza haitaruhusu maandamano ya aina yeyote.

Naye Kamishina wa kaunti ya Kilifi Joseph Keter ameonya wafuasi wa CORD wanaopanga kuandamana katika kaunti hiyo.

Keter anasema watakaoandamana watakabiliwa kisheria.

Kulingana na Keter wakaazi wa Kilifi wanapaswa kuyapa kipau mbele masuala yanayoleta utata katika kaunti hiyo.

“Hiyo maandamano haitafanyika Kilifi, na ikiwa kuna kiongozi anayeambia watu kutakuwa na maandamano kaunti nzima, tungeomba huyo kiongozi kwanza aongoze maandamano juu ya mashamba kuliko kufanya maandamano kuhusu IEBC. IEBC haihusu watu wa Kilifi inahusu Kenya nzima.” Alisema Keter.

Viongozi wakuu wa muungano wa CORD siku ya Jumapili walisisitiza kuwa maandamano ya Jumatatu yatakuwa ya amani.

Baadhi yao walidai kuwa baadhi ya viongozi wa muungano wa Jubilee walipanga njama ya kuzua vurugu katika maandamano hayo ili lawama ziendee CORD.

Maandamano yaliyopangwa Jumatatu, yanakuwa ya nne mfululizo licha ya polisi kutibua maandamano ya awali na watu kadhaa kujeruhiwa mjini Nairobi lakini CORD inasema wataendelea kuandamana hadi makamishna wa IEBC watakapo-ondoka ofisini.

Taarifa hii pia imechangiwa na Grace Mithamo

Comments

comments