Rais Kenyatta atenga shilingi bilioni moja kusaidia kilimo cha miraa

Rais Kenyatta atenga shilingi bilioni moja kusaidia kilimo cha miraa

by -
0 481
Fungu la miraa linapofungwa kabla ya kuuzwa. PICHA: HISANI

Nairobi, KENYA: Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa serikali yake itatenga shilingi bilioni moja katika bajeti ya mwaka ujao wa kifedha, kusaidia wakulima wa miraa.

Rais Kenyatta amechukua hatua hiyo kufuatia athari ambazo wakulima wa miraa wamepitia kufuatia hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya kupiga marufuku uuzaji wa miraa, katika mataifa hayo.

Miraa au ukipenda Mirungi, hutegemewa sana na jamii zinazoishi katika maeneo ya mashariki mwa mlima Kenya, ambao ni miongoni mwa watu wa jamii ya Wameru.

Sehemu zingine ambazo miraa imekuwa ikitumiwa sana ni Nairobi na Mombasa.

Raia amesema pesa hizo zitatolewa kupitia Wizara ya Kilimo.

Ametangaza hayo alipokuwa akitia saini kuwa sheria, mswada unaotambua mirungi kuwa mmea wa kulipatia taifa mapato.

Hii ina maana serikali sasa inaweza kuweka mikakati ya kutangaza, kuzalisha, kusambaza na pia kuuza zao hilo.

Rais Kenyatta ameongeza kuwa kutaundwa jopo kazi la kuangazia changamoto zinazokabili sekta ya ukuzaji wa miraa.

Jopo kazi hilo litatoa mapendekezo yake kwa serikali.

Inakadiriwa kuwa watu wapatao milioni 10 hutafuna mirungi kila siku kote duniani.

Comments

comments

SIMILAR ARTICLES