Watoto wa Lamu wakosa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio

Watoto wa Lamu wakosa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio

by -
0 348

Lamu,KENYA:Zaidi ya watoto 300 kutoka Wadi ya Basuba, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki, bado hawajafikiwa na chanjo ya ugonjwa wa kupooza-Polio, licha ya zoezi la utoaji chanjo hiyo kukamilika Jumatano wiki iliyopita.

Watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutoka vijiji vya Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe hawakuweza kufikiwa na chanjo hiyo baada ya maafisa wa afya wa kaunti ya Lamu waliokuwa wakitekeleza zoezi hilo la siku tano kudinda kwenda maeneo hayo kutokana na kile wanachodai kuwa ni kuhofia maisha yao.

Wadi ya Basuba imekuwa ikigonga vichwa vya habari kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab ambao wamekuwa wakitekeleza uvamizi wa mara kwa mara hasa kwa magari ya jeshi, polisi na hata yale ya abiria.

Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu, Dkt Mohamed Kombo, amethibitisha kuwa maafisa wake hawakuweza kufika kwenye vijiji husika, akisisitiza kuwa usalama eneo hilo bado ni wa ati ati.

Dkt Kombo aidha anailaumu idara ya usalama ya kaunti ya Lamu kwa madai kwamba ilikosa kushirikiana na idara yake katika kuhakikisha watoto wa Basuba wanapata huduma hiyo ya chanjo.

Comments

comments