Wahanga wa shambulio la kanisani Likoni waelezea kumbukumbu miaka miwili baadaye

Wahanga wa shambulio la kanisani Likoni waelezea kumbukumbu miaka miwili baadaye

by -
0 356
Waumini wa kanisa la Joy In Jesus Ministries miaka miwili iliyopita, saa chache baada ya shambulio. PICHA: WELDON KEMBOI

Likoni, KENYA: Waathiriwa wa shambulio katika kanisa la Joy in Jesus Ministries wilaya ya Likoni kaunti ya Mombasa miaka miwili iliyopita, wanaweza kukumbuka vyema yaliyojiri wakati watu waliokuwa wamejihami walipoingia kanisani wakati wa ibaada ya Jumapili na kuanza kufyatua risasi kiholela.

Sarah Adisa mama wa waototo watatu anakumbuka vizuri tukio hilo la tarehe 23 mwezi Machi mwaka wa 2014.

Sarah ambaye alikuwa na jukumu la kuwaelekeza wageni  hadi sehemu watakapoketi, anasema watu wanne waliokuwa wamefunika nyuso zao waliingia kanisani na kufyatua risasi huku wakisema nia yao ilikuwa ni kuwamaliza wote waliokuwa wakiendelea na ibaada.

“Niliketi katika kiti cha nyuma nikataka kuenda mbele pahali mume wangu alikua na watoto, nikapigwa risasi mbili mguuni.. nilijikakamua vilivyo na hapo nikamwona mume wangu amepigwa risasi kifuani na ikatokea mgongoni”, alisema Sarah kwa uchungu.”

Anasema alijaribu kumwita lakini alimkodolea macho huku akionekana kuhisi uchungu mwingi.

“Alipumua mara ya mwisho kana kwamba kuna jambo alitaka kutamka lakini hakuweza na hapo alikata roho. Alisema kwa huzuni na kwa uchungu.

Mwathiriwa huyo alisema alifanyiwa upasuaji na mabaki ya risasi ikatolewa, lakini maisha hayajakuwa rahisi kwake kwa kuwa alimpoteza mume wake ambaye alikuwa nguzo kwa familia yake.

Mwandishi wa Baraka Fm alipomuuliza endapo walikuwa na fununu ya shambulio kanisa hilo, Sarah alikimya kwa muda wa kama dakika moja hivi kabla ya kujibu.

“Mhhhh….siwezi nikajibu hilo kwa sasa lakini…..”,alitamka Sarah.

Mwathiriwa mwingine Diana Maloba, mama wa mtoto mmoja anasema alilazimika kutengana na mumewe baada ya shambulio hilo.

Bi Diana anasema alipigwa risasi tatu mguuni na mkononi huku mumewe akipigwa risasi tatu katika paja, mguuni na kiunoni.

Kuanzia siku hiyo Diana anasema ilibidi watengane na kila mmoja wao aishi na wazazi wake ili kupunguza gharama kwa kuwa wote walitengwa na rafiki zao kwa kuwa walikuwa wamelemaa.

Bi Maloba anasema alilazwa hospitalini kwa miezi sita  kitandani huku mumewe akilazwa  miezi minne.

Aliongeza kuwa amefaniwa upasuaji mara 11 kurekebisha mifupa iliyopasuliwa na risasi lakini bado anahitaji matibabu.

“Nilisikia mmoja wa watu hao akimwomba mwenzake risasi,na baada ya muda mfupi nikajipata  mlangoni nikiwa najiburuta nikiwa nimelala kifudifudi,”aliongeza Bi Maloba.

“Risasi moja imekwama kiunoni mwa mume wangu, na madaktari wanasema endapo itatolewa huenda akalemaa kabisa. Daktari alisema ni afadhali atumie dawa tu ili apunguze maumivu.” alielezea Bi Maloba.

Siku ya Jumapili waumini na viongozi walifanya ibaada maalum katika kanisa hilo la Joy in Jesus Ministies ambapo seneta wa Nairobi Mike Mbuvi aliahidi kulipia gharama ya shilingi laki mbili kwa waathiriwa hao wawili wanaotarajiwa kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya AIC Kijabe mjini Nairobi.

Japo idadi ya waumini imepungua katika kanisa hilo kwa asilimia kubwa, Bi Diana anasema hilo halitomzuia kuhudhuria ibaada kanisani.

Wakati wa shambulio hilo watu wanne waliuawa kwa kupigwa risasi huku wengine wakijeruhiwa.

Polisi haijatoa ripoti kuhusu ni nani aliyehusika ama ni kwa sababu gani kanisa hilo lilishambuliwa, japo kuliibuka taarifa kuwa wanamgambo wa al-shabaab walihusika.

Lakini kuna wale waliopuuza wakisema uvamini huo ulitokana na tofauti baina ya viongozi wa kanisa hilo.

 

Comments

comments

SIMILAR ARTICLES