Kesi inayohusu meli iliyolipuliwa baharini mwaka 2014 yaendelea mahakamani Mombasa

Kesi inayohusu meli iliyolipuliwa baharini mwaka 2014 yaendelea mahakamani Mombasa

by -
0 428

Mombasa, KENYA: Mashahidi wawili wametoa ushahidi mahakamani Mombasa kuhusu kesi dhidi ya raia 12 wa kigeni waliokamatwa bandarini Mombasa miaka miwili iliyopita kwa madai ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Shahidi wa kwanza ambaye ni afisa mkuu  katika maabara ya wizara ya madini Joram Wambua ameambia mahakama kuwa sampuli zilizotolewa katika meli zilibainika kuwa madini aina ya gypsum na kusema hazikuwa dawa ya kulevya.

Shahidi wa pili Wilfred Kagimbi ambaye ni meneja wa mamlaka ya masuala ya baharini, amesema hawezi kutambua vyema meli inayohusishwa na kusafirisha dawa za kulevya kwani hakupata fursa ya kuikagua.

Kagimbi amesema aliagiza wafanyakazi wengine wa cheo cha chini katika mamlaka hiyo kufanya ukaguzi.

Mashahidi wengine watano wanatarajiwa kutoa ushahidi Alhamisi.

Raia hao 12 kutoka Pakistan, India na Iran walikamatwa mwezi Julai mwaka 2014 bandarini Mombasa kwa madai ya kulangua dawa za kulevya aina ya  heroin na pia kumiliki  meli iliyosafirisha dawa hizo.

Mahakama ilielezwa kuwa walisafiri kutumia meli kwa jina AL NOOR iliyotia nanga  bandari ya Mombasa  mwezi huo wa Julai mwaka 2014 ikiwa na zaidi ya kilo elfu 35 za dawa za kulevya aina ya heroin za  thamani ya zaidi ya  shilingi bilioni moja.

Meli hiyo ililipuliwa mwaka 2014 ikiwa na dawa za kulevya kufuatia agizo la rais Uhuru Kenyatta.

Hapo nyuma kabla ya agizo hilo la rais, mahakama iliagiza meli hiyo isilipuliwe hadi kesi itakaposikizwa.

Mawakili wa washukiwa wakiongozwa na Gerald Magolo wameiomba mahakama  iagize waende bandarini kukagua meli inayodaiwa kusafirisha dawa hizo za kulevya kwa kuwa meli hiyo ingepaswa kutumiwa kama ushahidi katika  kesi hiyo.

Kiongozi wa mashtaka Alexanda Muteti hata hivyo amepinga ombi hilo  na kuambia mahakama hana ufahamu kuhusu sehemu ilikoegeshwa meli hiyo.

Hakimu Julius Nange’a ameagiza mawakili hao kuwasilisha ombi hilo Alhamisi.

Imehaririwa na Eliakim Mwachoni

Comments

comments