Wanafunzi 60 Mombasa Wafadhiliwa na Benki ya Equity.

Wanafunzi 60 Mombasa Wafadhiliwa na Benki ya Equity.

by -
0 444
Wanafunzi 15 kutoka Mombasa kisiwani na Likoni wakitabasamu kwa kupata "Wings To Fly" kufadhili elimu yao katika shule za sekondari.

Takriban wanafunzi 60 kutoka kaunti ya Mombasa watanufaika na mpango wa benki ya Equity maarufu kama ‘Wings To Fly’ ili kufadhili elimu yao katika shule za sekondari kuanzia mwaka huu wa 2016.

Wanafunzi hao ni wale werevu kutoka familia zinazolemewa kifedha kuwaelimisha watoto wao, waliopata alama zaidi ya 350 katika mtihani wa kitaifa wa darasa la 8 (KCPE) mwaka jana 2015.

Katika wilaya za Likoni na Mombasa Kisiwani wanafinzi 147 walituma maombi ya kufadhiliwa kupitia Wings To Fly, ndiposa bodi iliyotwikwa jukumu la kuwateua ikapata watahiniwa 15 walio na mahitaji zaidi.

Mwenyekiti wa bodi hiyo maarufu kama Community Selection Board  (CSB) Margaret Wandario alisema mchakato wa kuwateua hao 15 haukuwa rahisi, kwa sababu hata wengi waliokosa wana alama za juu.

Meneja wa benki ya Equity tawi la Moi Avenue mjini Mombasa Raphael Ngera aliambia Baraka FM kuwa walilazimika kutembelea familia za wanafunzi wengi, ili kubaini uwezo wao katika elimu kwa watoto.

“Wanachama wa bodi hii tulizuru boma nyingi na kuona jinsi watu walivyo na matatizo kama familia. Wengi hawajiwezi kugharamia elimu ya watoto hawa werevu, na hata wengine wanategemea wazazi wenye magonjwa mbali-mbali. Tunaamini Wings To Fly inawapa matumaini”, bwana Ngera alisema hayo katika mahojiano ya kipekee na Baraka FM.

Baadhi ya wanafunzi wanaofadhiliwa wameitwa kujiunga na shule za kitaifa, akiwepo Serena Joseph Otekwa aliyesomea shule ya msingi ya Star of The Sea na sasa atajiunga na shule ya kitaifa ya State House mjini Nairobi.

Mmoja wa wazazi aliyeshuhudia mtoto wake akitangazwa miongoni mwa wale wateule –Bi Shrini Aliasga aliambia Baraka FM kuwa hii ni zawadi kubwa kwa familia yake, wakati huu ambapo yeye anaugua saratani na mumewe hana uwezo wa kulipia watoto karo ya sekondari.

Mwaka huu wa 2016 mpango wa ‘Wings To Fly’ ulipokea maombi 22,000 kote nchini, na watakaofadhiliwa ni wanafunzi 2,000.

Wote watakongamana Ijumaa Februari tarehe 5 katika uwanja wa Kasarani mjini Nairobi katika hafla ya kila mwaka ya kuzindua ufadhili wa WINGS TO FLY, ukiwa ni ushirikiano wa Equity Group Foundation na The MasterCard Foundation.

Hafla hiyo itazunduliwa tena na rais Uhuru Kenyatta akiwa pamoja na mkurugenzi mkuu wa Equity Group James Mwangi.

Kufikia sasa takriban wanafunzi 500 wamefaidika kupitia programu ya uongozi chini ya Equity (ELP), na wengine kuajiriwa kazi kwa muda katika benki tofauti za Equity kote nchini hata kabla ya kujiunga na vyuo vikuu.

Wanafunzi 12 kati ya wote waliofadhiliwa kielimu walibahatika zaidi kujiunga na vyuo vikuu maarufu ulimwenguni, kama vile Yale na Harvard University nchini Marekani.

Comments

comments