Maweni Primary imekosa KCPE kwa miaka 37

Maweni Primary imekosa KCPE kwa miaka 37

by -
0 470
Shule ya msingi ya Maweni ilianzishwa mwaka wa 1979 lakini bado haitambuliwi na KNEC.

HOLA,KENYA:  Shule moja ya msingi kaunti ya Tana River iliyoanzishwa miaka 37 iliyopita haijawahi kuwa na mtahiniwa katika mtihani wowote wa kitaifa!

Shule hiyo MAWENI PRIMARY ilifunguliwa mwaka wa 1979 katika wilaya ya Tana River lakini ingali inasubiri kushuhudia mwanafunzi wa kwanza kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la 8 (KCPE).

Inashangaza kuona au kusikia kuwa shule hii ya Maweni ilianzishwa miezi michache tu baada ya kifo cha rais wa kwanza wa Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta, wakati huo mtihani wa kitaifa wa darasa la saba ukiitwa C.P.E.

Shule hiyo kwa sasa haitambuliwi na baraza la kitaifa la mitihani sawa na shule zingine kadhaa eneo hilo, kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi wanaopasa kufanya mitihani ya kitaifa.

Kamishina wa kaunti ya Tana River Isaiah Nakoru amewaonya wazazi na walezi wengine kutokana na hulka ya kuwaachisha masomo watoto.

Kamishna Nakoru alitoa agizo Jumatatu iliyopita kwa machifu na maafisa wengine wa utawala kuwasaka watu wanaokatiza elimu ya watoto kwa kuwaoza au kuwaagiza wachunge mifugo.

Pia aliwaonya wahudumu wa mabanda ya kuonesha fulamu akisema wanachangia kusambaratisha elimu eneo hilo.

Tana River ilikuwa miongoni mwa wilaya sita katika mkoa wa pwani na sasa ni moja kati ya kaunti 47 za Kenya, ikiwa na ukubwa wa kilomita 137,000 mraba.

Kwa mujibu wa sensa ya kitaifa ya mwaka 2009 Tana River ilikuwa takriban watu 240,100 ambao kwa wakati huu idadi hiyo inakisiwa kuwa zaidi ya robo-millioni.

Makao makuu ya Tana River ni mji wa Hola.

Comments

comments