Marais watatu waungana kuomboleza wanajeshi.

Marais watatu waungana kuomboleza wanajeshi.

by -
0 480
Marais Uhuru Kenyatta, Muhammadu Buhari na Hassan Sheikh Mohamoud wakiwa mjini Eldoret.

ELDORET,KENYA: Ibada maalum ya kuwa-enzi wanajeshi wa Kenya waliouawa na magaidi nchini Somalia Januari tarehe 15  ilifanyika Jumatano katika kambi ya kijeshi iliyo mjini Eldoret.

Ibada hiyo iliongozwa na wahubiri wa dini mbali-mbali na kuhudhuriwa na marais watatu: Muhammadu Buhari wa Nigeria, mwenyeji Uhuru Kenyatta, na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud.

Familia za wanajeshi waliouawa na pia waliojeruhiwa pamoja na wale wanaoendelea kulinda amani nchini Somalia zilihudhuria ibada hiyo, ambapo baadhi walipokea ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu kufuatia msiba wa kuwapoteza wapendwa wao.

Mamlaka ya Kenya imekawia kutangaza idadi ya wanajeshi waliouawa katika shambulio lililotekeelzwa na magaidi Januari tarehe 15, wakiwa katika kambi ya muungano wa majeshi ya AMISSOM eneo la El-Adde nchini  Somalia.

Mkuu wa jeshi la Kenya (KDF) Samson Mwathethe alilinganisha shambulio hilo na lile la mwaka 1998 katika ubalozi wa Marekani mjini Nairobi, akisema hili la El Adde lilikuwa karibu mara tatu kwa ukubwa.

Hata hivyo Kenya ina takriban wanajeshi 4,000 hasa kusini mwa Somalia, waliotikwa jukumu la kukabili kundi la Al Shabaab tangu mwaka wa 2011.

Katika hotuba yake mjini Eldoret rais Uhuru Kenyatta aliongoza marais wenzake kutoka Nigeria na Somalia kukemea tendo la ugaidi wa kimataifa, akisema muungano kama huo unawapa nguvu kukabili magaidi.

“Rais Buhari hapa na nchi yake Nigeria wanapitia mambo kama haya ambayo sio mageni kwao,sawa na sisi wanaomboleza kila wakati kwa sababu ya kushambuliwa na magaidi. Lakini hili linatupa ujasiri wa kupambana na mambo haya ya ugaidi,” alisema rais Kenyatta.

Marais Muhammadu Buhari wa Nigeria na Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia walitaja magaidi kama watu wasio na huruma, wakisema mitego yao yote itashindwa.

Wanajeshi wa Kenya ambao idadi yao bado haijabainika rasmi waliuawa pale kambi yao iliposhammbuliwa na magaidi, waliotajwa kama wanamgambo wa Al Shabaab kusini mwa Somalia.

Taarifa za karibuni zasema wakuu wa jeshi la AMMISSOM linalohudumu Somalia wametangaza mikakati zaidi ya kuwakabili magaidi wa Al Shabaab na washirika wao.

Wakati Kenya na Somalia wakisumbuliwa na wapiganaji wa Al Shabaab, Nigeria kwa zaidi ya miaka saba imehangaishwa na kundi la Boko Haram.

Comments

comments