Ushahidi : Feisal alichagua magari ya mizigo kusafirisha pembe za ndovu

Ushahidi : Feisal alichagua magari ya mizigo kusafirisha pembe za ndovu

by -
0 503
Feisal Mohammed akiwa katika mahakama maalum ya KWS Bamburi.

 

Ushahidi uliotolewa Jumatano mahakamani Mombasa kuhusiana na kesi ya ulanguzi wa pembe za ndovu inayowakabili washukiwa sita unaonyesha kuwa mshukiwa mkuu Feisal Mohammed, alikataa kusafirisha mizigo yake kwa kutumia magari yaliyo wazi.

Mashahidi watano wa kwanza katika kesi hiyo walisema mbele ya hakimu Diana Mochache kuwa Feisal alichagua magari yaliyofunikwa nyuma, akisema alikusudia kuhamisha mizigo ya nyumbani.

Mahakama ilipeleka kikao maalum katika kambi ya shirika la huduma kwa wanyama-pori (KWS) eneo la Bamburi mjini Mombasa ambapo mashahidi watatu walisikizwa Jumatano alasiri.

Shahidi wa kwanza Abdul Halim anasema alikuwa mtu wa kwanza kupigiwa simu na mshukiwa Feisal Mohammed akitaka gari aina ya Canter ili kusafirishiwa mizigo, na kwamba mbeleni aliwahi kumbebea sukari na mchele kwa malipo akitumia gari lake.

Shahidi mwingine Kassim Hassan Shughuli ambaye ni wakala wa kukodisha magari, aliambia mahakama kuwa Feisal alikataa kutumia gari lao kwa sababu halikufunikwa sehemu ya kubebea mizigo.

Kassim alichekesha kikao cha mahakama alipomwuliza wakili mmoja: “Mimi ukiniangalia naweza kweli nunua pembe za ndovu?”

Dereva aliyekuwa na gari hilo Seif Ahmed Mohamed naye anasema walikutana na Feisal eneo la Sparki mjini Mombasa akiwa pamoja na mshukiwa wa kwanza wanayemtambua kwa jina la Kaka.

Mashahidi hao walieleza mahakama kwamba washukiwa walikuwa na gari jeusi lililokuwa na nambari za usajili kutoka nchi ya Tanzania.

Shahidi wa tano Abdulrazak Omar ambaye gari lake hatimaye lilikubalika na kukodishwa na Feisal, aliambia mahakama kuwa alijihisi kusalitiwa baada ya gari lake kunaswa na polisi wa kitengo cha upelelezi, kwa kuhusiwha na biashara ya ulanguzi wa pembe za ndovu.

“Niliposoma magazetini kuwa amekamatwa niliingiwa na uoga sana nikijua serikali ikimfuata Feisal atanitia mashakani na mimi sikuwepo.

Twafunga swala sote katika msikiti wa Baluchi, kweli shetani hafuati mlevi,pepo yuko na anakujia kupitia kwa mtu mwungwana”, alisema Abdulrazak, mmiliki wa gari analosema alimkodoshia Feisal Mohammed.

Wakati wa kuhojiwa na mawakili sita walio katika kesi hiyo, Abdulrazak aliambia kikao cha mahakama kuwa amekosa kufanya biashara kwa miezi mitano kwa sababu gari linazuiwa na maafisa wa ujasusi.

Feisal Mohamed pamoja na washukiwa wengine 5 walidaiwa kulangua pembe za ndovu vipande 314 zilizonaswa katika bohari moja eneo la Tudor mjini Mombasa, Juni mwaka 2014.

Feisal alikamatwa nchini Tanzania Disemba mwaka huo wa 2014 na polisi wa kimataifa Interpol, na baadaye akasafirishwa Kenya ili kushtakiwa pamoja na washukiwa wenzake.

Wakili wa serikali Alexander Muteti anayewaongoza wanasheria wengine kuongoza mashtaka katika kesi hiyo, amesema wananuia kuwaita mashahidi 22.

Mahakama ya Mombasa ililazimika kuanza kusikiza upya kesi hiyo pale hakimu Diana Mochache alipoamua kulikuwa na mkanganyo katika nakala zilizochapishwa wakati kesi ikiendelea kusikizwa.

Awali hakimu Mochache aliagiza ofisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma kuwasilisha nakala zote wakati wa kuwahoji mashahidi.

Washukiwa wanawakilishwa na wanasheria sita kutoka Naiobi na Mombasa wakiwepo Gerald Magolo, Gikandi Ngibuini, na Moses Kurgat.

Baada ya kuwasikiza mashahidi 8 wa kwanza kikao cha mahakama kitazuru katika kituo cha polisi cha Urban, kukagua gari ambalo lilidaiwa kusafirisha pembe hizo za ndovu mwaka 2014.

Maafisa wa ujasusi wakiwepo wale wa shirika la KWS wameimarisha doria wakati kesi hiyo ikisikizwa katika kambi ya shirika hilo la huduma kwa wanyama-pori.

Nchi za Kenya na Tanzania zimeshuhudia ongezeko la wawindaji haramu wanaojihusishwa na ulanguzi wa pembe za ndovu na faru mweupe, kwa kuwaua wanyama hao kikatili.

Mataifa kadhaa ya bara Asia yanasalia soko kuu la baishara hiyo haramu.

Comments

comments