Rais Mteule wa Tanzania akabidhiwa cheti cha urais

Rais Mteule wa Tanzania akabidhiwa cheti cha urais

by -
0 574
Rais mteule wa Tanzania John Pombe Magufuli

Rais mteule wa jamhuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amekabidhiwa rasmi cheti cha urais kwa kushinda uchaguzi wa urais kuongoza jamhuri hiyo.

Magufuli wa Chama cha mapinduzi CCM amekabidhiwa cheti hicho pamoja na naibu wake mteule Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salam nchini Tanzania.

Mwandishi wa Baraka Fm Joseph Jira aliye jijini Dar es Salaam anasema ukumbi huo ulijaa hadi pomoni.

Magufuli alimshinda mpinzani wake wa chama cha Chadema chini ya muungano wa Ukawa Edward Lowasa katika uchaguzi ulioshuhudia upinzani mkubwa.

Alipata jumla ya kura milioni 8.8 huku Lowasa akipata zaidi ya kura milioni 6.

Magufuli sasa atakuwa rais wa 5 kuongoza jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Tanzania NEC Jaji mustaafu Damian Lubuva aliongoza hafla hiyo ya kumkabithi Magufuli cheti hicho.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo rais mstaafu wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye ni mwenyekiti wa Jumuia ya Madola.

Aliyekuwa akigombea urais wa chama cha ACT Ann Elisha Mgwira amemtaka rais mteule John Magufuli kuhakikisha anatetea usawa wa jinsia pamoja na kuirekebisha katiba.

“Badiliko la kwanza ambalo ninaliona na la msingi kabisa tunataka katiba mpya, tunataka katiba inayotokana na maoni ya wananchi ili itupe uhalali wa mabadiliko mengine tunayotaka kuyaona, tunahitaji kuona umoja wa kitaifa, tunahitaji kuona usawa kati ya wanaume na wanawake,” alisema Bi.Mgwira.

Wengine waliogombea wadhifa huo wa urais wamesusia hafla hiyo.

Imehaririwa na Eliakim Mwachoni

Comments

comments

SIMILAR ARTICLES