#JuliusYego Aweka Rekodi ya Kenya Kurusha Mkuki

#JuliusYego Aweka Rekodi ya Kenya Kurusha Mkuki

by -
0 514

Wanariadha wa Kenya Julius Yego –bingwa wa michezo ya Jumuia ya Commonwealth, ameweka rekodi mpya ya kitaifa katika kurusha mkuki.

Yego maarufu kwa jina la utani “YouTube Athlete” aliandika rekodi mpya Jumanne usiku, aliposhiriki mashindano ya kimataifa ya “Golden Spike” katika Jamhuri ya Czech.

Yego alichukua nafasi ya kwanza katika mji wa Ostrava, kwa kurusha mkuki umbali wa mita 86.88.

Bingwa huyo wa Afrika na pia michezo ya Jumuia ya Madola mwaka 2014, amesema sasa ndoto yake ni kushinda dhahabu katika michezo ya Olympiki mwaka ujao wa 2016, mjini Rio de Janeiro huko Brazil.

Julius Yego hakuwa maarufu miaka 5 iliyopita, lakini alijitahidi kujifunza kurusha mkuki bila kuwa na kocha.

Alibandikwa jina la “You Tube” kwa sababu ya kusoma zaidi na kujifunza kurusha mkuki, kupitia mtandao wa You Tube.

Katika mashindano hayo ya Golden Spike mjini Ostrava huko Ulaya, mkenya mwingine Asbel Kiprop alimaliza wa pili katika mbio tofauti za mita 1,000.

Naye David Rudisha anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 800 ya dakika 1:40:91 alipata jeraha akishiriki mbio maalum za mita 600, na akalazimika kujiondoa baada ya umbali wa mita 150.

Katika mbio za mita 100m kwa wanaume Asafa Powell wa Jamaica alirejea uwanjani kwa vishindo, na kushinda kwa muda wa sekunde 10.04.

Mjamaica mwingine Usain Bolt alisisimua uwanja mjini Ostrava, aliposhinda kwa urahisi mbio za mita 200 kwa muda wa sekunde 20.13.

Comments

comments